Hatua 12 Za Uhakika Za Kujenga Utajiri Mkubwa Kwenye Maisha Yako.

KITABU; MTAALA WA UTAJIRI.

Kwenye bunge la bajeti ya serikali ya Tanzania kwa mwaka 2023/2024, Mbunge wa Jimbo la Ngara Ndaisaba George Ruhoro alikuwa mmoja wa wabunge waliochangia kwenye makadirio ya mapato na matumizi katika ofisi ya rais ikulu na ofisi ya rais menejimenti ya utumishi wa umma na utawala bora. Kwenye mchango wake, Mbunge Ruhoro aliitaka Serikali kuanzisha mtaala unaohamasisha utajiri kwa Wanafunzi ili wanapomaliza elimu yao wawe wameshazijua fursa za uwekezaji na waondokane na dhana ya kuamini kila Tajiri ni Fisadi au kuhisi Freemanson.

Mbunge Ndaisaba George Ruhoro alisema; “Imefika mahali kwenye Taifa letu Watanzania wanaishi kwa woga, nilitarajia kwenye Taifa letu tuwe na Mawaziri wanamiliki ndege ila hatuna, ni waoga, sasa matokeo yake tunajinyima fursa, Mtu akiwa Tajiri anaonekana Fisadi au Freemanson”

Niliposikia kauli hii ya mbunge, wazo lilinijia kichwani kwangu kwamba unakosekana mtaala mmoja unaoweza kumfundisha mtu jinsi ya kujenga utajiri mkubwa kwenye maisha yake. Wanafunzi wanakaa kwenye mfumo rasmi wa elimu kwa miaka isiyopungua kumi, lakini kwenye kipindi chote hicho, hakuna somo la utajiri ambalo wanafundishwa. Kitu pekee wanafundishwa kuhusu fedha ni jinsi ya kuzihesabu na jinsi ya kutunza kumbukumbu zake. Lakini jinsi ya kuzitafuta, kwa wingi na ukubwa, hilo somo halipo kabisa.

Na hapo ndipo changamoto kubwa inapoanzia na kupeleka taifa kuwa na wananchi wengi masikini na lenyewe pia kuwa masikini. Kwa kusukumwa na kauli ya Mbunge Ruhoro, ambayo imebeba ukweli mchungu, nimekaa chini na kuandika kila ninachojua kuhusu safari ya kujenga utajiri mkubwa kwenye maisha.

Na hapa ni mwongozo kamili, kwa matumizi binafsi ya mtu anayetaka kujenga utajiri kwenye maisha yake. Nimeandika kwa uzoefu binafsi, kuanzia yale niliyojifunza kwenye usomaji wa vitabu zaidi ya elfu moja kwenye maeneo ya maendeleo binafsi, mafanikio, hamasa na fedha. Pia nimetumia uzoefu wangu binafsi, ambapo niliweza kuanzia chini kabisa, nikafuata hatua ambazo nimeshirikisha kwenye mtaala huu na kuweza kujenga biashara zinazoniingizia kipato cha uhakika.

Zaidi nimetumia uzoefu ambao nimeupata kwa watu wengine ambao nimekuwa nawafundisha, kuwashauri na kuwasimamia katika kuanzisha na kujenga biashara zao pamoja na kufanya uwekezaji. Wengi walianzia chini kabisa na kwa kufuata hatua unazokwenda kujifunza kwenye kitabu hiki, wameweza kupiga hatua kubwa. Wapo walioanza wakiwa hawana kipato kabisa, lakini wakaweza kujitengenezea kipato wao wenyewe. Wapo ambao walianza wakiwa wameajiriwa na kipato hakiwatoshelezi, wakaweza kuanza biashara na hatimaye kuacha ajira na kuendelea na biashara ambazo ziliweza kuwapa kipato kikubwa kuliko ajira. Pia wapo ambao walikuwa na biashara ndogo ambazo zinawategemea wao moja kwa moja, lakini baada ya kufuata hatua hizi wameweza kujenga biashara zinazojiendesha zenyewe bila ya kuwategemea moja kwa moja.

Eneo jingine kubwa ambalo tumeweza kufanyia kazi kwa uhakika na kupata matokeo mazuri kwa kufuata hatua hizi ni la uwekezaji kwenye masoko ya mitaji. Mimi binafsi niliujua uwekezaji wa vipande kupitia mfuko wa UTT mwaka 2013 na hapo hapo nikachukua hatua ya kuwekeza. Mwaka 2014 niliandika makala kwenye mtandao ninaoendesha unaoitwa AMKA MTANZANIA nikiwashauri watu wafanye uwekezaji kwa hatua ndogo ndogo kwenye mfuko huo na kujipa muda mrefu wa uwekezaji kukua. Wengi hawakuipa uzito makala ile, lakini wachache waliofanya hivyo wamepata manufaa makubwa. Kwenye programu zangu za ukocha ninazoendesha, kuwekeza UTT ni moja ya sharti la lazima kwa mtu kutimiza. Na kwa kutimiza sharti hilo, mpaka kufika mwezi Julai 2023, jumla ya uwekezaji uliofanywa na watu waliopo kwenye programu hizo ni zaidi ya shilingi Bilioni moja za Kitanzania.

Kwa sasa tupo kwenye mchakato wa kujenga utajiri wa zaidi ya dola bilioni moja kwa kila aliyepo kwenye programu hizo za ukocha ninazoendesha. Mchakato huo unaitwa Bilionea Mafunzoni ambapo tunafuata hatua hizi ambazo nimeziainisha kwenye kitabu hiki cha MTAALA WA UTAJIRI. Tunazifuata hatua hizi kwa msimamo bila kuacha. Na kwa historia ya kila mmoja wetu ya kule alikotoka na alikoweza kufika sasa, tuna uhakika wa kulifikia lengo hilo la ubilionea. Tunachofanya ni kufuata hatua hizi kama zilivyo na kwa ubora zaidi bila kuchoka wala kukata tamaa na kuishia njiani.

Nikukaribishe kwenye kitabu hiki cha MTAALA WA UTAJIRI, ukisome, ukielewe na kutekeleza haya unayokwenda kujifunza. Hiki siyo kitabu cha kusoma mara moja na kuwa umemaliza, bali ni kitabu cha kuambatana nacho kwenye safari yote ya maisha yako yaliyobaki hapa duniani. Ni kitabu cha kurejea mara kwa mara kwenye hatua unazochukua za kujenga utajiri mkubwa kwenye maisha yako.

Maarifa unayokwenda kuyapata kwenye kitabu hiki yana nguvu kubwa na yameonyesha mafanikio makubwa kwa wengine, yanaweza pia kukupa mafanikio makubwa. Hilo litawezekana kama tu utachukua hatua ya kuyafanyia kazi kwa msimamo bila kuacha. Katika kutekeleza maarifa haya utakutana na changamoto mbalimbali, lakini hilo halipaswi kuwa mwisho wa safari yako. Kwa kuendelea kufanyia kazi hatua hizi, utapata njia ya kuvuka kila changamoto na kufikia lengo lako la kujenga utajiri mkubwa kwenye maisha yako.

Mgawanyiko Wa Kitabu.

Kitabu hiki cha MTAALA WA UTAJIRI kina hatua 12 za kufuata ili kuweza kujenga utajiri mkubwa kwenye maisha yako, kulinufaisha taifa letu na kudumisha utajiri huo vizazi na vizazi. Hatua hizo 12 zinapaswa kufanyiwa kazi kwa pamoja na siyo moja baada ya nyingine. Kwani zote zinaungana pamoja kuleta matokeo makubwa ya utajiri ambao mtu anautaka.

Hatua ya kwanza ni kujenga mtazamo sahihi wa utajiri. Huwa hatuoni kitu jinsi kilivyo, bali jinsi tulivyo sisi wenyewe. Mambo yote unayojua sasa kuhusu utajiri siyo uhalisia ulivyo, bali ni kutokana na mtazamo ambao umekuwa nao. Kwa kuanza kuboresha mtazamo wako kuhusu utajiri unakuwa umefungua macho yako na kuiona dunia kwa namna ya tofauti kabisa. Ni lazima uanze kubadili mtazamo kabla ya kuendelea na safari ya kujenga utajiri.

Hatua ya pili ni kutumia muda wako vizuri. Muda ndiyo rasilimali yenye ukomo na uhaba mkubwa. Muda ndiyo maisha yako. Kila kitu kwenye maisha yako kinaathiriwa na jinsi unavyotumia muda wako. Kwenye safari yako ya kujenga utajiri, eneo la kwanza unalopaswa kuwa na udhibiti mkubwa nalo ni matumizi ya muda wako. Jinsi unavyotumia muda wako ndiyo itaamua kama utakuwa tajiri au masikini. Kwa kudhibiti na kutumia muda wako vizuri, utaweza kujenga utajiri mkubwa kwenye maisha yako. Hata kama utaanzia chini kiasi gani, kwa kujipa muda wa kutosha kwenye kufanyia kazi hatua hizi, hutabaki pale unapoanzia.

Hatua ya tatu ni kutengeneza kipato. Fedha ndiyo mbegu kuu ya kuzalisha utajiri mkubwa kwenye maisha yako. Na fedha yenye nguvu ya kukuwezesha kujenga utajiri mkubwa ni ile unayokuwa umeitengeneza mwenyewe. Hatua hii inaonyesha jinsi mtu yeyote yule aliye hai anavyoweza kuanzia popote alipo na kuanza kutengeneza kipato.

Hatua ya nne ni kuweka akiba. Utajiri haujengwi kwa kile ambacho mtu anapata, bali kile anachobakiza kwenye kipato anachoingiza. Kuweka akiba ni hatua muhimu ya kujenga utajiri baada ya kuweza kuingiza kipato. Hii ni hatua ambayo imekuwa ngumu kwa wengi na kuwa sababu ya wao kubaki kwenye umasikini. Kwa sababu kila mtu kwenye kipindi cha maisha yake kuna kipato anaingiza, lakini anaishia kutumia chote na kutokubaki na akiba. Kwa kuweka akiba kwenye kila kipato, mtu anaweza kujenga utajiri mkubwa.

Hatua ya tano ni kudhibiti matumizi. Kuweka akiba kumetangulia kudhibiti matumizi kwa sababu ili uweke akiba, lazima matumizi yawe madogo kuliko kipato. Lakini hapa kuna mtego, kama ukiingiza kipato unaanza na matumizi kisha inayobaki ndiyo unaweka akiba, kamwe hutaweza kuweka akiba, kwa sababu matumizi huwa hayaishi na kipato huwa hakitoshelezi. Kuondokana na hilo, unaanza kuweka akiba kwenye kila kipato chako, kisha kinachobaki ndiyo unatumia. Na kama kinachobaki hakitoshelezi unadhibiti matumizi yako na kuendelea kuongeza kipato chako.

Hatua ya sita ni kudhibiti madeni. Madeni yamekuwa shimo ambalo linawaweka watu wengi kwenye umasikini ambao hauishi. Tabia ya kuwa na matumizi makubwa kuliko kipato inapelekea watu kuingia kwenye madeni, ambayo yanafanya kipato kuzidi kutokutosheleza. Watu wanapoingia kwenye madeni, huwa yanaenda yakikua na kuwazamisha zaidi. Kudhibiti madeni ni hatua muhimu ya kufanyia kazi ili kuondoka kwenye umasikini na kwenda kwenye utajiri. Na hatua hii imeitwa kudhibiti madeni na siyo kuondoka kwenye madeni, kwa sababu madeni pia ni moja ya nyenzo za kujenga utajiri. Hivyo utajifunza madeni mazuri ya kuwa nayo ili kukusaidia kwenye safari yako ya kujenga utajiri.

Hatua ya saba ni kujenga biashara. Hii ndiyo njia kuu ya kujenga utajiri kwa sababu ni kupitia biashara ndiyo mtu unaweza kuingiza kipato kikubwa na kisichokuwa na ukomo, bila ya wewe kuwepo moja kwa moja. Njia nyingine za kuingiza kipato zinakuwa na ukomo kwa sababu zinakutegemea wewe. Kujenga biashara kubwa kunakupa uhuru wa fedha na muda na hivyo kukuwezesha kufikia utajiri wa kweli. Kwenye hatua hii utajifunza jinsi ya kujenga biashara kubwa na inayokuweka huru.

Hatua ya nane ni kufanya uwekezaji. Wakati kufanya biashara ndiyo njia kuu ya kujenga utajiri mkubwa, kufanya uwekezaji ndiyo njia kuu ya kutunza utajiri huo ili kudumu kwa muda mrefu. Uwekezaji ndiyo njia ya kuweza kuingiza kipato bila ya kufanya kazi moja kwa moja. Kwenye hatua hii utajifunza jinsi ya kuanza kuwekeza mara moja hata kwa kiasi kidogo kabisa.

Hatua ya tisa ni kutumia nyenzo. Rasilimali ulizonazo zina uhaba, kuzitegemea hizo peke yake huwezi kujenga utajiri mkubwa. Unahitaji kutumia rasilimali za wengine kwenye safari yako ya kujenga utajiri. Kwenye hatua hii utakwenda kujifunza nyenzo kumi unazopaswa kuzitumia ili kuweza kujenga utajiri mkubwa unaotaka kuufikia.

Hatua ya kumi ni kuyakabili mabadiliko. Safari ya kujenga utajiri mkubwa siyo wa njia iliyonyooka, kuna mabadiliko mbalimbali ambayo utayapitia. Kina vikwazo na changamoto mbalimbali ambazo utakutana nazo. Ikiwa hujajiandaa, utakwama kwenye safari hiyo, kama ambavyo wengi wanaishia kukata tamaa. Hatua hii itakupa mikakati ya kuweza kukabiliana na mabadiliko yoyote unayokutana nayo kwenye safari ya kujenga utajiri ili kuikamilisha bila kuishia njiani.

Hatua ya kumi na moja ni utajiri wa taifa. Taifa tajiri linajengwa na wananchi ambao ni matajiri. Sisi kama wananchi tuna wajibu wa kuhakikisha tunachangia kwenye kulifanya taifa letu kuwa tajiri. Lakini pia uongozi wa taifa una majukumu yake ya kukamilisha ili kuleta mazingira mazuri kwa kila mtu kufanyia kazi na kufikia lengo la utajiri. Hatua hii itakupa majukumu hayo ya pande zote na jinsi yanavyotegemeana ili kuwa na wananchi matajiri na taifa tajiri pia.

Hatua ya kumi na mbili ni kutawanya utajiri. Hadithi za utajiri ambao baadhi ya watu wameteseka maisha yao yote kuujenga huwa hazina mwisho mzuri, hasa pale aliyejenga utajiri anapofariki dunia. Nyuma anaacha familia na ndugu wakigombania mali na hata kupoteza utajiri wote ambao umejengwa. Hatua hii inakupa mikakati ya kufanyia kazi ili utajiri unaoujenga uendelee kuwa na manufaa kwa watu wengi hata baada ya wewe kufariki dunia.

Kwa kuzielewa hatua hizi 12 za MTAALA WA UTAJIRI, na ukazifanyia kazi huku ukijipa muda, utaweza kujenga utajiri mkubwa na wa uhakika kwenye maisha yako.

Shukrani.

Shukrani za dhati ziwafikie wote ambao wamekuwa wananufaika na maarifa ambayo nimekuwa nashirikisha kwenye programu mbalimbali za mafunzo ninazoendesha kupitia mitandao ya AMKA MTANZANIA, KISIMA CHA MAARIFA na BILIONEA MAFUNZONI.

Wafuatao ni baadhi ya wanufaika wa mafunzo ambayo nimekuwa natoa na ambayo mengi ndiyo sehemu ya mtaala huu wa utajiri;

Alex Kamata, Alfred Mwanyika, Ali Khamisi, Awadhi Mjaka, Basil Danghalo, Beatus Elias, Bosco Mlomo, Christian Shoo, Christina Luambano, Christopher Mwijage, Claudio Mwambene, Cosmas Medson, Daniel Zake, Datius Deus, Deogratius Kessy, Deodatus Kessy, Dickson Mollel, Didas Mwombeki, Elihuruma Nnko, Emanuel Maitarya, Emanuel Mcharo, Emmanuel Mwakakuka, Enelisa Mbwile, Ernest Paschal, Fabiab Filemon, Faraji Kitonge, Farhia Omar, Felician Meza, Felix Rumisha, Frank Kandugu, Frank Mapunda, Freddy Ndolezi. Fum Jaffar, Godfrey Mbise, Godius Rweyongeza, Hassan Abdulla, Helanane Ilomo, Hendry Lema, Hillary Chuwa, Huvira Peterson, Innocent Kavishe, Isaack Zake, Jackson Mbilinyi, Jofrey Sanga, John Magori, Juma Lusewa, Jumanne Ndorobo, Kelvin Kinyaga, Kizito Bakwanye, Laurence Leon, Leonard Amo, Martin Tindwa, Maureen Kemei, Miraji Luwi, Mseco Kidee, Mustapha Kunyaula, Notbruga Basili, Nyamizi Simbachawene, Palmo Ulomi, Pascal Kasanda, Patson Chaula, Petro Kangalawe, Ramadhani Samizi, Raphael Macha, Rashidi Mpande, Regina Panga, Reinfrid Maganga, Rejoyce Otaru, Sebastian Kalugulu, Sebastian Moshi, Selemani Mbwambo, Simeon Shimbe, Stanslaus Kashinje, Wade Kibadu, William Loma na Yusuph Yusuph.

Utasoma shuhuda za baadhi ya watu hao kwenye hatua ya nyongeza iliyo mwisho wa kitabu hiki na kuona jinsi maarifa haya yalivyo na nguvu pale yanapofanyiwa kazi kwa uhakika.

JINSI YA KUPATA KITABU CHA MTAALA WA UTAJIRI.

Kupata nakala yako ya kitabu cha MTAALA WA UTAJIRI ili uweze kujenga utajiri mkubwa na wa uhakika kwenye maisha yako, wasiliana na namba 0678 977 007.

Karibu usome kitabu hiki na kukifanya kuwa sehemu ya safari yako ya kujenga utajiri mkubwa kwenye maisha yako.

Kocha Dr. Makirita Amani,

www.utajiri.tz